
Wabunge nchini Rwanda wamepitisha
mswada utakaoidhinisha kubadilishwa kwa vipengee vya katiba
vitakavyoruhusu rais Paul Kagame kuongoza kwa muhula wa tatu.
Katika
kipindi cha miezi kadhaa iliyopita mamilioni ya raia nchini Rwanda
wamekuwa wakitia sahihi pendekezo la kumtaka rais Kagame kuendelea
kuongoza taifa hilo hata baada ya kukamilika kwa muhula wake wa pili.
Kupitishwa
kwa mswada huo sasa kunatoa fursa ya kufanyika kwa kura ya maoni ya
iwapo ni haki kuruhusu uongozi wa zaidi ya mihula miwili au la.
Rais Kagame mwenyewe amesema kuwa huo utakuwa ni uamuzi wa raia wa nchi hiyo wenyewe.
Wanaharakati wa kupigania haki za kibinadamu wanasema kuwa utawala wa
Rwanda unakandamiza uhuru wa kujieleza na hivyo kunyamazisha vyombo vya
habari na upinzani.
Iwapo kura hiyo ya maoni itafaulu basi sheria
itakuwa imefungua mlango kwa rais Paul Kagame kuwania hatamu ya tatu
mwaka wa 2017.
Rais Kagame alichaguliwa kwanza katika mwaka wa 2003.