
Wanamgambo wa Al Shabaab wamesema
kuwa ni wao waliotekeleza shambulizi Kaskazini Mashariki mwa Kenya
ambapo watu 14 waliuawa usiku wa kuamkia jumanne.
Shambulio hilo linaaminika kuwalenga wafanyikazi wa machimbo ya mawe wasiokua wenyeji wa mkoa huo.
Walioshuhudia wamezungumza kuwa walisikia mwanzo milipuko miwili kisha ikafuatiwa na milio ya risasi.
Shirika la msalaba mwekundu linaongoza oparesheni ya kuwaokoa majeruhi ambao idadi kamili haijulikani .
Nani washambuliaji ?
Wanamgambo wa Al shabaab wamekuwa wakilenga wakaazi wasio wenyeji wa asili katika eneo hilo katika mashambulio yaliyotangulia.
Shambulio
kama hilo dhidi ya wachimba migodi lilitokea jijini Mandera mwezi
Disemba 2014, ambapo takriban watu 36 waliuawa na wengine wengi
kujeruhiwa.
Marudio ya shambulio
Mashambulio
kama haya yametishia kudumaza shughuli za maendeleo na kiuchumi katika
eneo la Kaskazini Mashariki mwa Kenya ambapo wengi wa wafanyikazi wake
ni watu kutoka maeneo mingine ya Kenya.
Wafanyikazi hawa wamekuwa wakidai kutishiwa maisha, na wengi wa
wafanyikazi kama vile walimu na hata wahudumu wa afya wamesusia kurejea
kazini katika eneo hilo wakidai kutishiwa maisha yao.
Chini ya
siku kumi zilizopita serikali ya Kenya iliondoa marufuku ya kutoka nje
kuanzia magharibi hadi alfajiri, kufuatia wito kutoka kwa viongozi wa
kiislamu waliodai kuwa marufuku hiyo inahujumu ibada za waislamu za
usiku katika mwezi wa Ramadhani.
Asili mia kubwa ya wakaazi katika eneo la kaskazini mashariki mwa Kenya, ni waislamu wa asili ya kisomali.